Kazi inapozidi, mwanadamu huumia kwa mawazo na kukosa muda wa kupumzika. Wapo baadhi ya watu ambao huelekea ufuoni mwa ziwa au bahari kubarizi. Ni Patulivu Ziwani


Ni Patulivu Ziwani

Baridi ndiyo hapana, njoto iwapo majini,
Utulivu huwiana, kubarizi ufuoni,
Huwa mengi ya kufana, asubuhi na jioni,
Ni patulivu ziwani, penye upepo mwanana.

Huko mengi mwakumbana, yawayo na ya kubuni,
Ya kuudhi ndo hakuna, kuna mengi ya makini,
Haikosi kuzozana, tena si haba ‘tamani,
Ni patulivu ziwani, penye upepo mwanana.

Kutoka kazi mchana, Jumapili kanisani,
Uwapo na jema dhana, ama utake makani,
Yapo mengi ya kuvuna, yasiyo na walakini,
Ni patulivu ziwani, penye upepo mwanana.

Tena muda kujivuna, pamwe nao wapendani,
Mwendapo mkalumbana, si raha mnathamini,
Hata kichwa ukakuna, mwisho utajiamini,
Ni patulivu ziwani, penye upepo mwanana.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*