Wakati mwingine matukio huwa ni kinyume kabisa kuliko tunavyotegemea. Tunapoiona ishara ya mvua, si lazima mvua ikanyesha. Hivyo basi, tusiliweke tumaini kwa jambo moja tu, huenda ukafa moyo linapokosa kutimia. Si Lazima Itanyesha


Si Lazima Itanyesha

Ni dalili ya mvua, yawapo juu mawingu,
Ila moyo huumbua, yakiangua utungu,
Sifate unayojua, usipatwe malimwengu,
Hili wingu likitanda, si lazima itanyesha.

Yapo yawapo yasiwe, huenda yasitimie,
Kisikwingie kiwewe, nayo hofu iwadie,
Matukio uyajuwe, usojua lififie,
Hili wingu likitanda, si lazima itanyesha.

Hata iwe watabiri, haliwi shuruti kuwa,
Mengine yataghairi, iwe hali kutenduwa,
Kama watakavyokiri, ni balaa na beluwa,
Hili wingu likitanda, si lazima itanyesha.

Huenda likafanyika, kama lipo lisemwalo,
Heri ulitie shaka, ukalidhani lisilo,
Lijapo likakufika, si lazima lifikalo,
Hili wingu likitanda, si lazima itanyesha.

Liwate la tegemezi, tenda usilolitenda,
Ukamwachie Mwenyezi, pekee asiyedinda,
Yadhihirike ya wazi, ushindapo ukashinda
Hili wingu likitanda, si lazima itanyesha.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*