Wakati mwigine huwa tunakosa maneno ya kutosha kuwaambia tuwapendao. Tunapokosa kuwapasha, huonekana kama tumewapuuza tu. Kwa beti tano tu hapa, ujumbe umefika. Una Mengi Kupendeka


Una Mengi Kupendeka

Umetenda, la mahaba ukanipa,
Umelinda, la hofu ukalitupa,
Hujakwenda, nalo deni ukalipa,
Umetenda, ewe wangu maridhia.

Wayataka, mazuri ya kupendeza,
Umetaka, yanayofukuza kiza,
Umefika, wendako ukaongoza,
Wayataka, tena yasiyo na shari.

Umedinda, wengine ukahujumu,
Umeshinda, wewe ndiwe wa kudumu,
Hujaranda, wengine wakuhukumu,
Umedinda, ukawa wa kupendeka.

Limetanda, wingu jema la amani,
Limewanda, likakosa walakini,
Umeunda, jina lisilo kifani,
Limetanda, likawa kielelezo.

Yatazame, yajayo ya kuwadia,
Iandame, nyota kukuangazia,
Lisikwame, bali likakufikia,
Yatazame, mengi uliyotimiza.

Maoni 2 ya “Una Mengi Kupendeka”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*