Je, ni wema gani umewahi kumtendea mwenzako? Je, ni wema gani ambao utakumbukwa nao? Litazame shairi hili linaowasifu kina mama wa neema. Kina Mama wa Neema


Kina Mama wa Neema

Alivyokuwa Debora, nitatumikia Mungu,
Nitahubiri ubora, wa neno jema la Mungu,
Hakuogopa Debora, alivyonena ya mbingu,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Kisa cha Esther twajua, Biblia tumesoma,
Mwombezi alivyokuwa, kwa enzi alivyovuma,
Hata mimi nitatua, sala kwa Mungu kutuma,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Na kama Abigaili, mimi nitanyenyekea,
Watumishi nitajali, miguu kuwaoshea,
Nitafanya kila hali, hisani kuwatendea,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Kama Hannah wa imani, wanangu nitaongoza,
Niwalete kanisani, Mwenyezi kumtukuza,
Mungu wanapomwamini, neno hawatapuuza,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Priscilla mwamjua, kwa kitabu cha matendo,
Neno alifafanua, kwa walio na upendo,
Ni hivyo nitaamua, kufunza walio kando,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Kwa mjane mshunami, Mungu nitatumaini,
Sivunjiki moyo mimi, nina Mungu maishani,
Ya mashaka siandami, Mungu ndiye nathamini,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Nitakuwa kama Lydia, kumtukuza Mwenyezi,
Wema nitawafanyia, wa kanisa viongozi,
Nitawakaribishia, nyumbani kwangu i wazi,
Daima nitajifunza, na wamama wa Neema.

Tabitha mwenye hisani, wengi alisaidia,
Mavazi aliyabuni, na watu kuwapatia,
Alifaa maskini, wote waliofifia,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Joanna alivyokuwa, kwa fadhili tena wema,
Fedha zangu nitatowa, kusaidia huduma,
Hakika nimeamuwa, kujitolea daima,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

Maria aliamuwa, yatendeke kwake mema,
Mfano linavyokuwa, neno lake la hekima,
Ni muhimu kulijuwa, neno la Mungu ni jema,
Daima nitajifunza, na wamama wa neema.

© Kimani wa Mbogo (04/07/2019)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*