Umetenda, la mahaba ukanipa,
Umelinda, la hofu ukalitupa,
Hujakwenda, nalo deni ukalipa,
Umetenda, ewe wangu maridhia.
Wayataka, mazuri ya kupendeza,
Umetaka, yanayofukuza kiza,
Umefika, wendako ukaongoza,
Wayataka, tena yasiyo na shari.
Umedinda, wengine ukahujumu,
Umeshinda, wewe ndiwe wa kudumu,
Hujaranda, wengine wakuhukumu,
Umedinda, ukawa wa kupendeka.
Limetanda, wingu jema la amani,
Limewanda, likakosa walakini,
Umeunda, jina lisilo kifani,
Limetanda, likawa kielelezo.
Yatazame, yajayo ya kuwadia,
Iandame, nyota kukuangazia,
Lisikwame, bali likakufikia,
Yatazame, mengi uliyotimiza.
Shairi bora la mahaba.
Umefikiria sana ndio maana ukaleta kitu kizuri sana