Kasuku unavyobwata, sikio umelitega,
La kugeza hujasita, huna la kukutitiga,
Ya wengine hukuvuta, mabingwa ukawabwaga,
Unavyopenda kuiga, kutwa moja utajuta
Hadharani kajileta, ushupavu kwa mabega,
Huna jambo la kutweta, kutisha walo kwa uga,
Unavyopenda kuiga, kutwa moja utajuta!
Unapania kupita, ila bado wakufuga,
Ungekuwa umekita, wangekutwaa kwa mbuga,
Gwiji unavyojiita, mfawidhi takuaga,
Unavyopenda kuiga, kutwa moja utajuta
Jitenge nayo ya kwata, wajuao takumega,
Dunia inakusuta, hujiwezi kama figa,
Huigi bingwa kuketa, hata kavalia njuga,
Unavyopenda kuiga, kutwa moja utajuta!
Huwi fundi kwa kuota, kifaranga ukataga,
Mahiri ukijiita, si kifua kujipiga,
Wajuao kufuata, hutendi kumagamaga,
Unavyopenda kuiga, kutwa moja utajuta!