Maana ya Ushairi

Shairi ni tungo yenye muundo na lugha ya kisanii na inayofuata utaratibu wa vina na mizani, hisi au tukio juu ya maisha au jambo na hufuata utaratibu maalumu wa urari na muwala unaozingatia kanuni za utunzi.

Ushairi ni sanaa ya kutunga mashairi kwa madhumuni ya kutumbuiza au kuelimisha. Shairi lililotungwa lazima liwe na maudhui na dhamira kwa kusudi la kupasha ujumbe. Kama kazi nyingine za fasihi, mshairi hutumia tamathali za usemi na wahusika ila ana uhuru wa kutumia lugha ilmuradi azingatie kanuni za ushairi.

Mgogoro umekuwepo kati ya wanamapokeo na wanamabadiliko kuhusu maana ya shairi. Wanamapokeo (wanajadi) wakisisitiza kuwa vina na urari wa wa mizani ndio msingi wa Ushairi wa Kiswahili. Wanamabadiliko (wanamapinduzi), ambao ndio washairi wa kisasa, nao wakidhibitisha kuwa si lazima shairi liwe na vina na urari wa mizani ili liitwe shairi la Kiswahili.

Mashairi yana umuhimu wa kipekee katika jamii kama ifuatavyo:

 1. Kuibua hisia za kuburudisha na kuhuzunisha
 2. Kukosoa, kukashifu na kubadilisha tabia zisizofaa katika jamii
 3. Kupasha ujumbe  kwa hadhira kwa njia ya mvuto
 4. Kuelimisha, kuhamasisha na kuzindua jamii
 5. Kuhifadhi matukio muhimu ya historia ya jamii
 6. Kuhifadhi na Kuendeleza Utamaduni
 7. Kukuza Ushujaa, Ujasiri na Uzalendo
 8. Kufikirisha na kunoa fikra
 9. Kuliwaza
 10. Kuonya, kutahadharisha, kunasihi na kuelekeza
 11. Kuadilisha na Kuadibisha
 12. Kusifia mtu au kitu
 13. Kuendeleza na kukuza kipawa cha utunzi
 14. Kupamba, kukuza na kuineza lugha
 15. Kuhifadhi msamiati wa lugha ya Kiswahili na Sanaa ya fasihi
 16. Kuburudisha hadhira na wasomaji
 17. Kukejeli au kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya jamii
 18. Kuwasilisha hisia za ndani za mtu na mawazo