Jiji lenye washairi, waghani, wajuzi, wachambuzi na waneni. Ni jiji gani hili? Jiji Langu, Jiji Gani?


Jiji Langu, Jiji Gani?

Mghani 1
Nakupa huu wajibu, kwa shairi nimeghani,
Jiji lenye uratibu, Waswahili wamo ndani,
Twavithamini vitabu, jiji letu la amani,
Naomba unipe jibu, jiji langu jiji gani?

Mghani 2
Ninakuomba ruhusa, nikujibu kwa makini,
Jiji lako ni Mombasa, huko ni Uswahilini,
Huko kuna vingi visa, kusoma ni yao fani,
Hakukosi madarasa, kwa jiji lako la Pwani.

Mghani 1
Si Mombasa jiji hili, halikosi burudani,
Jiji lenye njema hali, jiji langu la waneni,
Hutahitaji nauli, kufika kwangu jijini,
Naomba yako kauli, jiji langu jiji gani?

Mghani 2
Huenda ni Nairobi, nchi yetu ndilo mboni,
Ameliwezesha Rabi, nasi tunalithamini,
Mashariki Magharibi, nimetazama ramani,
Nimekujibu hababi, jiji kuu la hisani.

Mghani 1
Nairobi haliwezi, jiji langu la madini,
Lina wengi wachambuzi, na halikosi waghani,
Kunao wengi wajuzi, wasiofanya utani,
Wahitaji uchunguzi, jiji langu jiji gani?

Mghani 2
Jiji lako Zanzibari, jiji bila ubishani,
Lugha kwenu ni johari, kwenu basi visiwani,
Kuna wengi washairi, tungo zao twabaini,
Watu wenye umahiri, huko kwenu Ujombani.

Mghani 1
Sitajibu kwa faragha, jibu langu hadharani,
Sitaki iwe balagha, jibu langu hukudhani,
Kwetu twaikuza lugha, kwa Kiswahili twabuni,
Jiji ni Nuru ya Lugha, kipindi cha redioni.

Mghani 2
Nashukuru nimejua, nimetia maanani,
Nuru ya lugha twatua, toka bara hadi pwani,
Jibu lako ni murua, hakika nimeamini,
Twaja mengi kutambua, daima tusikizeni.

© Kimani wa Mbogo (20/03/2023)

Katika shairi hili la ngonjera kati ya Mghani 1 na Mghani 2, tunaweza kuona jinsi lugha ya Kiswahili inavyotumiwa kwa ubunifu katika kuwasilisha ujumbe. Mghani 1 anauliza jiji lake ni lipi, na Mghani 2 anajibu kwa kutaja majina ya miji mbalimbali nchini Kenya na Tanzania. Baada ya majibizano haya, Mghani 1 anafichua kuwa jibu lake ni Nuru ya Lugha. Hii inaonyesha umuhimu wa kukuza lugha yetu ya Kiswahili na kuitumia kama chombo cha kuelimisha na kuburudisha jamii. Shairi hili ni mfano mzuri wa jinsi lugha inavyoweza kutumika kwa ubunifu na kujenga umoja katika jamii.

Maoni 1 kwa “Jiji Langu, Jiji Gani?”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*