Haramu Hii Imani

Nanga ninang’oa sasa, natunga kuwaaseni, kuhusu mpya imani,
Imani inawanasa, hasa walo maskini, huwaletea mapeni,
Mapeni yakawakwasa, wanaishi kasrini, Rabuka kutoamini,
Haramu hii imani, hupoteza waja wengi, wasiotoa kafara.

Nyote mpendao pesa, sikiliza kwa makini, haramu hii imani,
Imani itakutesa, utabaki maskini, usipotii kanuni,
Kanuni takunyanyasa, faida zake huzuni, utarudi mavumbini,
Haramu hii imani, hupoteza waja wengi, wasiotoa kafara.

Imevisheheni visa, ajali bararani, haramu hii imani,
Imani ina vipusa, wenye miili laini, mafisi huwaamini,
Huwaamini kabisa, nao huzama penzini, mwishowe wasiamini,
Haramu hii imani, hupoteza waja wengi, wasiotoa kafara.

Ya mengi yake mikasa, imani hii gizani, hutumbukiza shimoni,
Shimoni huna fursa, kurudi kwake Dayani, utaungua motoni,
Motoni huna ruhusa, kutamani ya mbinguni, utateseka jamani,
Haramu hii imani, hupoteza waja wengi, wasiotoa kafara.

© Lawrence Gaya