Ya dunia yasikutishe. Tena usijidai na ulicho nacho. Usione una mali tele ukawadharau wengine. Jua wapo wenye mali na hadhi. “Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.” Huna Hadhi Huna Haki

Huna Hadhi Huna Haki

Hunalo la kujinaki, ila lako kutulia,
Dhiki baada ya dhiki, tena wingi wa udhia
Mwanadamu ku, zidi kujinyamazia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Ukata utakuteka, bila la kufurahia,
Kuyumba na kuudhika, ndilo lako kubakia,
Mateso kutaabika, tena wingi kuumia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Tenda lako likufae, tena iwe njema nia,
Bahati ikatandae, hata kama yafifia,
Tena vema unyamae, wengine kuangazia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Usijione kujua, wengine wajijulia,
Ama la kujifutua, na debe kujipigia,
Chunguza na kutambua, dunia yanotukia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Unasema una mali, makubwa kujitakia,
Itazame yako hali, ujue yakikujia,
Ulijue la ukweli, uwe wajifahamia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Hata ua hunyauka, chini kujiangukia,
Tena hufa wanowika, kuwahusu hufifia,
Dunia hukugeuka, ukabaki kuumia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Usijidai kujua, usijute na kulia,
Ya ulimwengu tambua, ujue yanowadia,
Yalo mafumbo fumbua, kwa mema ukajitia,
Huna hadhi huna haki, ina wenyewe dunia.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*