Uko wapi mpaka wa mbaya na mwema? Nani anayependeza na asiyependeza? U wapi mpaka? Palikuwa…


Palikuwa…

Palikuwa mwizi, kuku akaiba,
Palikuwa jizi, gari likaiba,
Palikuwa kijizi, sindano kaiba,
Yupi aseiba?

Palikuwa na kichwa, bulibuli vaa,
Palikuwa jichwa, jitunga kavaa,
Palikuwa kijichwa, kidongea vaa,
Yupi asevaa?

Palikuwa mdudu, mtu akauma,
Palikuwa dudu, ndovu likauma,
Palikuwa kidudu, mwenzake kauma,
Yupi aseuma?

Palikuwa mtoto, machozi kalia,
Palikuwa toto, lita likalia,
Palikuwa kitoto, tone likalia,
Yupi aselia?

Palikuwa njia, jeshi likapita,
Palikuwa na jia, madovu kapita,
Palikuwa kijia, siafu kapita,
Ipi isopitwa?

© Kimani wa Mbogo (01/01/2009)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*