Kokoriko sijaimba, ningali sijawa nyuni,
Makanyagio yayumba, ukubwa sina sinani,
Sidonoi hata tumba, henitoshi kidonani,
Subiri niwe mtamba, kifaranga nafaani?
Najizoesha kutamba, mwewe selea angani,
Wanisaka kwa kizimba, miye wanitakiani?
Hujaola yangu gumba, uniache salimini,
Subiri niwe mtamba, kifaranga nafaani?
Jimbi umekuwa mamba, unimege udogoni,
Wanivuta twende chemba, unidone faraghani,
Usinifunge kwa kamba, unitwae mafichoni,
Subiri niwe mtamba, kifaranga nafaani?
Kikwara unanikemba, udogo wangu huoni,
Wahaka umenikumba, nikuonapo chumbani,
Kuenda kwenye shamba, wanifata u mbioni,
Subiri niwe mtamba, kifaranga nafaani?
Kunifata wanitimba, uniache mchangani,
Kama ngozi waniwamba, uchafu unisheheni,
Hishimu aleniumba, nitotolewe yaini,
Subiri niwe mtamba, kifaranga nafaani?
© Kimani wa Mbogo (15/04/2010)