Waajiriwa wana mengi yanayowaudhi kutekeleza wajibu wao. Wengine hutumiwa tu na mabosi wao kama chombo cha kuwatajirisha angaa wapate riziki. Mwajiriwa atatumia muda wake hata wa ziada ili bosi apate mapato kwa wingi. Lakini si wengi hutambua juhudi za waajiriwa hao. Malipo ni mishahara duni, kunyimwa haki, kubekuliwa na kubaguliwa. Ni mja yupi hupenda kuona akinyanyaswa ama haki zake zikikosa kuheshimiwa?

Kwenye shairi hili, chungu kimetwikwa jukumu la kunena. Kinalalamika kwamba mpishi hukitumia tu kumtimizia haja zake za mapishi. Chungu kinalinganishwa na mwajiriwa anayeteswa. Chungu kitatumika usiku na mchana ila mpishi hapakui chakula akakipa hata tonge. Chungu hiki pia kinaweza kulinganishwa na mwanamke nayetumiwa tu na mwanamume kumtimizia haja za kimapenzi bila kupata chochote.

Shairi hili la Kimani wa Mbogo liliibua hisia tofauti kati ya wasikilizaji wa redio ya QFM mwaka wa 2010 lilipoangaziwa kwenye kipindi cha Rashid Abdalla na Lolani Kalu kilichoitwa Hekaya za Mswahili. Chungu Naungulika Nisile


Chungu Naungulika Nisile

Mafiga umeyapanga, mekoni kuniinjika,
Kuni umeshazipanga, kwa moto ukaniweka,
Nyinginezo wazichonga, moto wako kuukoka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Asubuhi uwe nami, staftahi kupika,
Kuniunguza hukomi, wadhani sitoudhika,
Una bahati sineni, nichomwe sitosikika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Chungucho sipumziki, upike nami kishuka,
Wadhani siunguliki, chakula chako nataka,
Wanigota sitamki, kwa mwiko unapopika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Hutoniacha jioni, chajio unakitaka,
Upike umenihini, chungu sitotambulika,
Ukigawa hunioni, kinakwisha cha kulika,
Miyechungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Usiku nimo motoni, wache supu kuchemka,
Kila wakati kazini, sina pa kupumzika,
Hunitii maanani, tamaa ikanitoka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Mpishi hunao wema, siati kunung’unika,
Hujaona nimegoma, kaziyo kutofanyika,
Wataka yangu huduma, ukipata watoweka,
Miyechungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Mfinyanzi alianza, motoni akaniweka,
Mpishi wa kunitunza, moto sijanusurika,
Kila wakati kukanza, mwenyewe hunufaika,
Miyechungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Vigae hutovitaka, mwenyewe nikivunjika,
Kila siku nateseka, wewe ukisaidika,
Motoni naungulika, ubaki wafurahika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Sizikosi haki zangu, hili likaeleweka,
Usije nitia pingu, mambo yako ukitaka,
Wadhani sina uchungu, motoni kuungulika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Asubuhi u nami, unitumie kishuka,
Jioni umejihami, kwako kazi kufanyika,
Kazi zangu hazikwami, chakula bado chalika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Masinzi tonge hayawi, bado sijaliwazika,
Kwangu katu hayaliwi, yakawa yanamegeka,
Nisemapo sisikiwi, majukumu wanitwika,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Kujihami ni lazima, maneno nikatamka,
Nimeamua kugoma, chakula kutopikika,
Hamnalo la huruma, kwenye raha kuniweka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

Hainitishi kejeli, hadi langu kusikika,
Nitabaki na la kweli, ili niwe natukuka,
Watazama yangu hali, udongo ukiucheka,
Miye chungu nachomeka, nisipate hata tonge?

© Kimani wa Mbogo (01/01/2010)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*