Tunapoisherehekea siku ya wanawake duniani, kumbuka huyo mwanamke aliyejitolea kwa bidii zake zote ili uwe ulivyo leo. Mama Ninakupongeza

Mama Ninakupongeza

Mama leo nakuwaza, si haba nimebaini,
Kwa shairi nakutuza, nikusifu duniani,
Ulimwengu naeleza, wajue nakuthamini,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Kunibeba uliweza, miezi tisa tumboni,
Kwa siha ukajikaza, ukiwa na tumaini,
Sikuwa wa kuchukiza, nawe hukunilaani,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Mwenyezi Mungu Muweza, kanileta duniani,
Mama ukaniongoza, u mwalimu maishani,
Mema kanielekeza, hisani kanisheheni,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Uliweka kiambaza, nibaki na ya imani,
Nikajua pa kucheza, tena pa kuwa makini,
Mwana hukubembeleza, kawa sina walakini,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Hakika hukudekeza, ya hekima ukabuni,
Ya siri ulichunguza, mazuri ukitamani,
Ulikemea ya kiza, potofu kuwa laini,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Mamangu hukunibeza, ulifanya ya amani,
Ukawa wanicharaza, nikitenda yalo duni,
Imani kaniagiza, niyafuate ya dini,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Mama hukunipuuza, nikawa najiamini,
Mengi ulinikataza, mema niliyodhani,
Kila siku kutangaza, uyapendayo moyoni,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Ulizidi kupendeza, kama waridi kondeni,
Hakika uliangaza, ukawa nyota angani,
Wema uliendeleza, ikatawala hisani,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

Mama kamwe hukuzoza, wala kuwa na utani,
Kuonya hukunyamaza, faragha na hadharani,
Mema ulisisitiza, yatendwayo duniani,
Mama ninakupongeza, una mengi ya thamani.

© Kimani wa Mbogo (08/03/2023)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*