Unapomtafuta mwandani, heri kuwa makini na kuchunguza mienendo yake. Huenda ukajifunga pingu na atakayekuwa mateso kwa maisha yako yote. Mke Mjuaji


Mke Mjuaji

Kheri ‘siwe bibi katu, heri sifunge nikahi,
Hakika usidhubutu, kisema kwako futahi,
Kumwoa mjuvi mtu, hilo wazo lifusahi,
Kheri sifunge nikahi, kheri na usithubutu.

Kumuoa mjuaji, heri tokwa roho bila,
Popote utamkaji, takuwa wake kwa hila,
Daima ugeuzaji, usemayo kwa sahala,
Kheri kumuoa fala, badala ya mjuaji.

Kumua mjeuri, kwako mwingi ukalifu,
Daima atahitari, dawamu ni usumbufu,
Yeye ni mwenye ushari, huyo wa ubadilifu,
Hupati ukubalifu, umwoapo mjeuri.

Kamwe sioe mjuvi, usodai wake mwingi,
Kumwoa mke mjuvi, ni utadi wake mwingi,
Simuoe wa ujuvi, Kisicho fupa hafungi,
Uneni wake mwingi, simwoe mke mjuvi.

Lolote akwambialo, hilo hutamtafiri,
Lolote alitendalo, bila ya kutabasuri,
Lolote alifanyalo, tafanya kwa ujeuri,
Kama hatatahayari, kwa lolote afanyalo.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2007)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*