Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu na kulisifu jina lake. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Wimbo Nitacheza


Wimbo Nitacheza

Nina wajibu kusifu, Mungu nikamsifia,
Ya sifa nimuarifu, kwa nyimbo nikimwimbia,
Lazima nikamsifu, muda umeshawadia,
Wimbo mimi nitacheza, Mwenyezi nimchezee.

Mapema nitaamka, vema nijitayarishe,
Wimbo nitauandika, sifa njema nizipashe,
Hilo nimewajibika, lazima nihakikishe,
Kayaba nitachukua, Mwenyezi nikamsifu.

Ngoma kubwa nichukue, iliyowambwa kwa ngozi,
Madhabahuni nitue, niuanze utangazi,
Mkwiro niuchukue, niidunde kwa ujuzi,
Ngoma nitaidunda, muziki mwema nicheze.

Rahima nitamsifu, kwa kutumia gitaa,
Niianze tawasifu, nyuzi sita kuandaa,
Nimtukuze Latifu, kote muziki kujaa,
Gitaa nitachukua, kwa vidole niicheze.

Vizuri nitasimama, tarumbeta kupuliza,
Nicheze kwa taadhima, vali nikizibonyeza,
Nitamsifu Rahima, sifa zake kutangaza,
Tarumbeta nipulize, wimbo wangu nimwimbie.

Wimbo wangu utavuma, madoido nitatia,
Maneno mazuri mema, kwa wimbo nitamwimbia,
nitacheza kwa hishima, sifa nikampatia,
Wimbo mimi nitacheza, Mwenyezi nimchezee.

Maoni 1 kwa “Wimbo Nitacheza”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*