Hili ni shairi lililotungwa 2018. Mshairi akiwauliza wenzake kuhusu lugha ya mtaa kwa jina Sheng. Sheng’i Dude Gani?

Sheng’i Dude Gani?

Babu wa Ujarumani, ninalo nataka juwa,
Lanisakama bongoni, sijapata kuelewa,
Sijajuwa asilani, mawazo napungukiwa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Hamisi wa Marekani, iwapo umegunduwa,
Amba nondoke kizani, fikira ziweze tuwa,
Nifahamishe tungoni, wajinga ndio huliwa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Mchiriza sumu ghani, tuweze ipata dawa,
Hino janga li jijini, Kiswahili laumbuwa,
Toka bara hadi pwani, lugha yetu yaunguwa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Walibora Marekani,changiya niweze juwa,
Nyote nifahamisheni, fahamu nije ingiwa,
Kitumiwacho jijini, vijana kawa wajawa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Mbogholi nakuawini, langu lije fikiriwa,
Liandikwe nyarakani, nami niwe kaelewa,
Silitaki la utani, la makini nimejawa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Naja kwako Athmani, hisani nije fanyiwa,
Fahamu yangu i duni, mema sijakabidhiwa,
Sitotaka unihini, ukweli kuufichuwa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Mwamboga miye sikani, ukweli sijaambiwa,
Tunga hata liwe guni, nipate kukuelewa,
Sinalo li ubongoni, kwa ujinga navamiwa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

Gikambi nielezeni, sitaki kusailiwa,
Kariri au ughani, ukweli nije ujuwa,
Nieleze kwa udani, busara sijajaliwa,
Nipashe nije ng’amuwa, hino sheng’i dude gani?

© Kimani wa Mbogo (01/10/2008)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*