Ninalitazama jiji, lenye wingi kupendeza,
Wahandisi kwa vipaji, matajiri kuwekeza,
Majumba yaliyopangwa, kama haya ya kuumbwa.
Usafi na usafiri, wa mfano kupigiwa,
Mandhari ya bahari, ndiyo bora kusifiwa,
Mpangilio dhabiti, jiji linalopendeza.
Nchi kavu na angani, wasafiri waridhika,
Kandawala yu makini, waendako wakafika,
Hili jiji lina mema, wakazi wafurahia.
Milimani kuna watu, mabondeni hawakosi,
Uzuri wao ni utu pasipo na la uasi,
Ni jiji lililo jema, wema usio kifani.
Wema wa hali ya hewa, tena inayovutia,
Si jua na si mvuwa, hewa ya kufurahia,
Jiji linalopendeza, linalo wingi wa sifa.
Hamna la ukabila, uraia ndio hoja,
Yapo muhimu maswala, ya kunufaisha waja,
Mji bora kwa watu, uishi na kuwekeza.
Utawala ndio mwema, jiji hili kushamiri,
Duniani unavuma, kwa zake njema habari,
Jiji linajulikana, kwa sifa kadha wa kadha
Keep it up