Usimbeze mwenzako kwa sababu ya jambo la kufikiria. Ni vema kulitafiti kwanza kabla ya kuamua. Huenda ukajipata kwa maafa usipochunguza jambo kabla ya uamuzi. Masingizio Siyataki


Masingizio Siyataki

Ya nyumbani na ya siri, hao wanakupa yani?
Na wasema ni dosari, mambo yangu ya kanuni,
Nao hao wafikiri, yatamfaidi nani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Wasikiza wadadisi, na kunipuza kwa nini?
Kumbe hao wajasusi, kwa kweli ni wafitini,
Habari za wafilisi, sikio watega lani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Njiani we wanipita, na vidomo kimya kwani?
Kuongea unakata, ati hutaki uneni,
Kufanya mambo kutata, ndiko kuwa ufanani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Wasema nimekufuru, wanidhulumia nini?
Uniache niwe huru, siutaki ubishani,
Na kamwe usinizuru, utanizuru kwa nini?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Matendo kanuni yangu, yanakusakama kwani?
Tumekuwa nao kwangu, takwimu nyingi nyumbani,
Kuwakosoa wanangu, waniulizia yani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Kosa ni langu wasema, nimemkosea nani?
Na ikiwa ni Karima, basi sio kanisani,
Kwa mwana nitubu hima, yakini mzazi nani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Maneno kwa kusanjari, waniingilia kwani?
Usinitakie shari, kwa Mola ni barakani,
Waniambia nikiri, dhambi wapi walakini?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Leo waniangazia, kosa kalipata lini?
Ila wanitafutia, wabagua yangu sini,
Yote kwa kupindukia, ubaguzi nao wani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Sababu dinari sina, ndio maana utani?
Kwa madhahabu naona, dinari ndiyo hisani,
Wale dinari hawana, hawatapasi langoni?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*