Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii. Ataitwa Mnazarayo


Ataitwa Mnazarayo

Ameposiwa Mariamu, na Yusufu mwenye haki,
Nalo jambo la muhimu, jambo Yusufu hataki,
Ana mimba Mariamu, Yusufu atahamaki,
Haya yote twayasoma, nyarakani takatifu.


Ni malaika kwa ndoto, anamwambia Yusufu,
Atampata mtoto, Mariamu asihofu,
Si ajabu hilo pato, ni Roho Mtakatifu,
Usihofu kwa lolote, haya yote yalinenwa.

Yeye atazaa mwana, jinale Imanueli,
Yeye ni Mungu maana, Pamoja nasi kwa kweli,
Huyo mwana mwenye jina, aokoe bila swali,
Yusufu umsharifu, huyo mwana ni mfalme.

Mamajusi wamkafika, toka kwao mashariki,
Kumuona wakitaka, huyo mwenye kibariki,
Herode kafadhaika, hilo jambo halitaki,
Ataka yeye pekee, ukuu aumiliki.

Bwana wapi azaliwa, Herode akauliza,
Papo hapo kajibiwa, kishaye wakimweleza,
Bethilehemu azawa,ufalme tapoteza,
Nayo hii ni taarifa, ikampa hangaiko.


Mwokozi amezaliwa, himaya yote ni yake,
Atakayebarikiwa, na Maulana babake,
Heri atakayekuwa, akiyaamini yake,
Nauliza langu swali, ndaniyo amezaliwa?

Herode akawatuma, wale mamajusi wote,
Akawaamuru hima kutafuta Kristo kote,
Herode kwa taadhima, kumshujudu apate,
Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti.

Wakaongozwa na nyota, hadi alikozaliwa,
Kristo dhahabu kapata, uvumba pia akawa,
Manemane,kwa kitita, zile zote akapewa,
Hizi zote ni zawadi,alipewa mfalme.

Mungu naye kawajia, Mamajusi kama ndoto,
Mungu akawaambia, yeye hataki mtoto,
Wasiende yake njia, ataka afe mtoto,
Wale wote mamajusi, wakapitia nyingine.

Yusufu kawachukua, Mwokozi na mama yake,
baada ya kutambua, kutoka kwa mola wake,
Herode ataamua, hataki Mwokozi kwake,
Wakaelekea Misiri, na kukaa kule wote.

Herode lipofariki, wakaandamana wote,
Mwana-Herode kabaki, himaya naye apate,
Naye mwenye kubariki, Nazareti akupate,
Manabii walinena, taitwa Mnazarayo.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*