Wakati mwingine binadamu hufika mwisho na kuvunjika moyo akitazama hujuma, ubaguzi na mateso yanayomkabili. Wengine hujiua na wengine husumbuka katika maisha yao yote bila msaada kwa wafadhili. Nataka Nife


Nataka Nife

Kule wananishutumu,
Wale watanitahemu,
Wote watanihasimu,
Niache nataka nife!

Hao hawana huruma,
Leo wale ni husuma,
Wale waso taadhima,
Niache nataka nife!

Kuhasimiwa siendi,
Kutehemia siendi,
Kuhujumiwa siendi,
Niache nataka nife!

Kule mema siyapati,
Huduma njema sipati,
Huko chema sikipati,
Niache nataka nife!

Kule nitahasimiwa,
Najua sitatibiwa,
Kifo nitahukumiwa,
Niache nataka nife!

Upuuzi siutaki,
Mie naitaka haki,
Nataka ustahiki,
Niache nataka nife!

Wauguzi ni wahuni,
Waganga ni wafitini,
Wahazigi ni watani,
Niache nataka nife!

Siendi kwa wauaji,
Kwa haki wapokaji,
Wao si ualisaji,
Niache nataka nife!

Wasio nyoyo kunjufu,
Wasio uangalifu,
Wasio uaminifu,
Niache nataka nife!

Walio na uhalifu,
Walio uharibifu,
Walio na udhaifu,
Niache nataka nife!

Wasio ubainifu,
Wasio uchangamfu,
Wasio na ufanifu,
Niache nataka nife!

Siutaki ubaguzi,
Siutaki upuuzi,
Siutaki ubekuzi,
Niache nataka nife!

Ukabila siutaki,
Urafiki siutaki,
Uhongaji siutaki,
Niache nataka nife!

Asilani sendi kwao,
Kamwe sikitaki chao,
Katu silitaki lao,
Niache nataka nife!

Siniambie lolote,
Leo siendi kokote,
Kwa Rabana nigute,
Niache nataka nife!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*