Kuna baadhi ya wazee ambao hawapendi kamwe kuitwa wazee. Wangali bado hawajakubali kuwa uzee umewateka nyara na watotako kwa ujana hawarudi kamwe. Usimwite Nyanya


Usimwite Nyanya

Ndiye malikia, katika budhara,
Kwake dhukuria, sana kudorora,
Kwao ingilia, mpango dharura,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Mwenye ikirari, na mkubalifu,
Mwenye kudamiri, na mharibifu,
Chake ni kiburi, na mbadhirifu,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Kwama mhadhiri, wa chuo kikuu,
Kawa umahir, kapewa ukuu,
Kanza kudamiri, wale vitukuu,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Kawa mpashaji, alo redioni,
Kenda tangazaji, mwenyewe sokani,
Kawa payukaji, kapasha ya soni,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Kawa mhadhiri, pwani taasisi,
Kule kashamiri, kote kuramisi,
Kawa na aheri, baada kuasi,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Katu hajisetiri, atenda ujana,
Tupu kanchiri, hadharani ana,
Huyo wa nadhari, kapenda ujana,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Sije mwite nyanya, aliye rubani,
Wengi awakanya, katu si utani,
Wengi akusanya, kuenda rahani,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Huyo wa elimu, si haba alopata,
Benzi gurudumu, liendalo tata,
Nao kwa kaumu, mwombea ukata,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Huyu kazeeka, myaka themanini,
Chumvi abugika, kuwa uzeeni,
Ila atukuka, kote budharani,
Usimwite nyanya, tajihatarisha.

Maoni 2 ya “Usimwite Nyanya”

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*