Wapo waotunga mashairi lakini jambo ni kwamba, wanatumia njia inayofaa? Washairi itawalazimu kukaa chini na kuzua mbinu zitakazoilinda fani hii kabla ya kuungua. Fimbo Niambie

Fimbo Niambie

Edita nibakizie, nafasi ya kuandika,
Mnyonge niulizie, anijibu kwa hakika,
Pia umchapishie, jibu lake ninataka,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Fimbo nihakikishie, utenge zako dakika,
Dhahiri uniambie, nijibu kwa kuandika,
Mada yangu uchangie, tuweze kukaramka,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Ushairi tuutie, utamu kuongezeka,
Washairi waingie, ukumbini kwa haraka,
Ushairi tupigie, kura nyingi kwa hakika,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Usinyamaze nambie, usinipuze andika,
Kampeni tuanzie, tuweze kuongezeka,
Mbinu gani tutumie,ushairi kuinuka,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Ladha nyingi tuutie, siagi jemu kupaka,
Kisha tuwakirimie, waja wote kwa haraka,
Uhondo wafurahie, ushairi kutukuka,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Nyumbanu weaambie, ushairi kutukuka,
Baitini nipashie, washairi kuinuka,
Nyumaye tusibakie, tumalize yangu shaka,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Tafadhali nitungie, mbinu ya kuvumaina,
Mengi tukawafanyie, wanyonge wadhoofika,
Swali langu nijibie, jibu lako kusikika,
Ya mnyonge niambie, tufanyeje kwa hakika?

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*