Upungufu wa kinga mwilini ni jambo lililowatesa wengi. Hadi sasa, jambo hili limewaua wengi na wengine kuacha bila tumaini na maisha, kiasi cha kwamba kifo tu ndicho hatima. Bara la Kifo


Bara la Kifo

Mkongwe baba na mama, dada kwa na kaka zanguni,
Tuungane kwa heshima, tuepuke hatarini,
Bara la kifo kuhama, jangwani nduguzanguni,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Maisha huwa ni raha, mwishowe ni kaburini,
Iwapo wewe yu juha, basi sikiza makini,
Haliistahi jaha, hili janga si jubuni,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Makala kwa magazeti kuhusu janga someni,
Naye ambaye hapati, redioni sikizeni,
Upate msamiati, ndivyo uhame jangani,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Walimu wetu shuleni, mawaidha jaribuni,
]Wanagenzi sikizeni, waadhi kwenu makini,
Nalo sikio tegeni, wanagenzi wenzanguni,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Mwendani wangu sikiza, isikize kwa makini,
Ngugu nakupendekeza, damu upimwe jamani,
Upate nakueleza, kujizuilia kifoni,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Kistaajabu ya Musa, taona ya Firauni,
hili janga kulinusa, twa kutia jenezani,
Mimi wewe changa pesa, marehemu kaburini,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Hili janga kukupata, lakutia hatarini,
Nacho kifo chafuata, unahama duniani,
Miti nayo twaikata, mbao hizo jenezani,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Sote tunakusanyika, pamoja huko nyumbani,
Watu wote kwa hakika, waomboleza kaburini,
bila yeyote kucheka, twakutia mchangani,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Ndugu yangu ewe nawe, uliye nao poleni,
Ukiwache hiki kiwewe, upendezwe na amani,
Maakuli mema yawe, afya nzuri jamani,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Nami nikitamatisha, niseme ndugu zanguni,
Kusema sio kutisha, yatilie maanani,
Nao ujumbe kupasha, kila taifa jamani,
Pamoja tuunganeni, bara la kifo tuhame.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*