Usinibague kwa hali yangu. Aliye na uwezo na kunijua sana ni Mungu aliyeniumba. Yawache yangu na ukome kunibekua! Ubekuzi Wa Nini?


Ubekuzi Wa Nini?

Katu siyacheke yangu, usiambe asiloani,
Na wanionapo tangu, mengi meamba lakini,
Sibekue yalo yangu, sibane kichinichini,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Zisokuwa zako pingu hizo wajitwika zani?
Ubekuzihuwa tangu, hali kuifanya duni,
Waonapo kazi yangu, wapita changaraweni,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Katu siyacheke yangu, kesho yangu huioni,
Hujui mpanga wangu, ulonileta kazini,
Kwao itakuwa chungu, wapita changaraweni,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Sibekue kazi yangu, msingi wake rubani,
Usiambe yalo yangu, mpango wangu huoni,
Sibague sura yangu, hunioni asilani,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Wapitao umbo langu, wapita changaraweni,
Kila siku sura yangu, wapata changaraweni,
Lakini mpango wangu, changaraweni huwoni,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Mambo mengi yalo yangu, ja uhondo wa junguni,
Hawoni silika yangu, isiyo ya kikosini,
Ufasaha ulo wangu, ja maji yalo mtoni,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Ile sime ilo yangu, iloning’inizwa vazini,
Hiyo ndo huona kwangu, wapita changaraweni,
Ubekuzi nao kwangu, niliyepita chuoni,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Uhusuo yalo yangu, ubekuzi ulo wani?
Katu siyacheke yangu, mpango wangu huoni,
Sibekue yalo yangu, kesho yangu huioni,
Ubekuzi ulo wani, uhusuo yalo yangu?

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*