Mtoto yatima hupitia mengi maishani. Wakati mwingine huona kama hajapendwa. Husononeka na kuudhika bila kuwa na kumfariji, Majonzi Daima

Majonzi Daima

Ninasikitika, ninasikitika, ninasikitika, 
Mimi nasikika, nikisikitika, leo kwa hakika,
Kweli bila shaka, na tama kushika, kwa kusikitika,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Mimi kwa ukata, konde nikipita, kaburi napata,
Moyoni natweta, kuona matuta, huku nikipita,
Baba alipita, mama akapita, hofu nikapata,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Kwa mpendwa mama, uliyenihama, haya ninasema,
Kaburinimama, sasa natazama, huku nainama,
Mwanao yatima, mimi sitakosa, kwona wako wema,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Tangu wewe kufa, mimi kwangu sifa, zawa kwa misafa,
Baada ya kufa, kwetu ni maafa, yasiyo ya sifa,
Ndoto kwa miswafa, zilizo za sifa, na zote zikafa,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Kwangu ni dhulumu, kwa kuhudumu, na kunihujumu,
Kila siku tumu, yaani saumu, wananilazimu,
Kwao hunikimu, walio waamu, ni kama kuzimu,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Moyo unatuta, huku kwa kutweta, nami kwa kujuta,
Mimi sijakita, wao waniketa, pale kwa ukata,
Ua nafumbata, toka kwa matuta, na kulichanyata,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Naliona ua, lililochanua, kaburi latua,
Moyo laumbua, na kuniungua, napolisekua,
Linanizuzua, kwa kuwachukua, na kunitandua,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Elimu sipati, amani, sipati, na haki sipati,
Wazazi hayati, wao vizingiti, walienda shoti,
Popote sipiti, mwanakibuhuti, mwana wa hayati,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Zigo wanitwika, mimi kwa dhihaka, bila kuongoka,
Mwili kuumuka, na kupepesuka, kwa kazi ya shaka,
Pigo wanitwika, kwa kughadhabika, matusi kufoka,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Mara nakumbuka, ya kale miaka, moyo naumbuka,
Raha kupomoka, ikapukutika, kifo kumunyaka,
Sitonung’unika, lakini baraka, kwangu zitanyoka,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Baba pia mama, laleni salama, huko kwa Karima,
lakini tazama, hali ya unyama, na ya kutandama,
Na yangu huduma, kwa wasio wema, wasio rehema,
Majonzi daima, na changu kilio, kote chasikika.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*