Tenzi ni tungo ndefu za ushairi zinazoelezea juu ya mambo fulani na huwa na pande moja katika utenzi wake (yaani huwa na vina vya Kati tu). Tenzi huweza kuwa na mpangilio wa silabi zinazolingana katika kila mstari pia haufuati urari wa mizani katika mshororo wake. Soma utenzi huu wa Lawaridi. Utenzi: Lawaridi


Utenzi: Lawaridi

(1).
Palikuwa na banati,
Huyo angaitwa siti,
Kitongojini Kahati,
Zama alipozaliwa.

(2)
Mtoto mwema ekuwa,
Wema ndio alijawa,
Maridadi alikuwa,
Urembo ukamjaa.

(3).
Sifa zake zilijaa,
Mtoto bila hadaa,
Hakuwa nazo fazaa,
Lawaridi angekua.

(4).
Si machache alijua,
Hana lilomsumbua,
Watuu hakuwaumbua,
Lawaridi alifana.

(5).
Kawa nalo jema jina,
Kwa marefu na mapana,
Mabaya aliyakana,
Mema akayakariri.

(6).
Mwana mwema wa Zuberi,
Lawaridi mwenye ari,
Akikosa alikiri,
Kikembe chake fukara.

(7).
Mtoto wa kibapara,
Aliyekulia bara,
Siku za vitimbakwira,
Aling’aa Lawaridi.

(8).
Alifwata itikadi,
Hakupenda ukaidi,
Alichukia utadi,
Rabuka alimwamini.

(9).
Kaenda jiji shuleni,
Akasoma kwa makini,
Asiupende utani
Akapendwa na mwalimu.

(10).
Wazee aliheshimu,
Kawapenda wanadamu,
Ghulamu kwa maharimu,
kuonyesha taadhima.

(11).
Likizoni alilima,
Kakishika kiserema,
Kifani cha mkulima,
Japo asingetamani.

(12).
Ngechaguliwa diwani,
Kaongoze mitaani,
Atamalaki jijini,
Japo kawa wasiwasi.

(13).
Alitamani saisi,
Awe harimu mwasisi,
Aliogopa farasi,
Hivyo basi hangekuwa

(14).
Kuli naye hangekuwa,
Aliogopa mabwawa,
Bandarini hangetuwa,
Afanyekazi ya kuli.

(15).
Angekuwa mhazili,
Taipu isiwe mbali,
Hakutaka kulihali,
Hakupenda ujuaji.

(16).
Angekuwa mwalisaji,
Kawadunge kwa siriji,
Hakupenda udungaji,
Aiumize miili.

(17).
Wakili alitamani,
Afanye mahakamani,
Aongoze sheriani,
Akatamani si haba,

(18).
Alimpongeza baba,
Udogo wake wa saba,
Alipopata msiba,
Kushindwa ngekuwa nani.

(19).
Walikuwa ukatani,
Bila hela mfukoni,
Angeendaje chuoni,
Achekwe sana na somo?

(20).
Kayatamani masomo,
Aufuate mfumo,
Huo wake msimamo,
Halambe waliandaa.

(21).
Walikomesha balaa,
Mashaka hizo nyakaa,
Mema yalitapakaa,
Karo walipochangiwa.

(22).
Furaha aliingiwa,
Lawaridi alijawa,
Banati kusaidiwa,
Ende akasome shule.

(23).
Angefikia kilele,
Shahada apate tele,
Korti apinge kelele,
Haki afuatilie.

(24).
Nchi yake ivutie,
Wakata ahudumie,
Mazuri awafanyie,
Haki ifuatilike.

(25).
Ndugu wa toka nitoke,
Jamaa waneemeke,
Chungu chema ainjike,
Nasaba kubahatika.

(26).
Shuleni alipendeka,
Hakuweza kuudhika,
Yake yalilainika,
Kwa bidii akasoma.

(27).
Akajawa na heshima,
Kafarijika mtima,
Akawa banati mwema,
Aliyepita shuleni.

(28).
Aliingia chuoni,
Lawaridi maskini,
Akasoma kwa makini,
Wavyele wakiteseka.

(29).
Chuoni kahishimika,
Wahadhiri kupendeka,
Huyo hakusawajika,
Urembo aubadili.

(30).
Mwanagenzi uwakili,
Sheria aibadili,
Mpaka Isirafili,
Ipulizwe parapanda.

(31).
Japokuwa alikonda,
Thamaniye ilipanda,
Unadhifu angeshinda,
Urembowa maumbile.

(32).
Kavuma kama mvule,
Walipojua lengole,
Sifa Zilikuwa tele,
Banati mkakamavu.

(33).
Huyo hakuwa mvivu,
Lawaridi mtulivu,
Ekuwa mvumilivu,
Mabivu kayatafuna.

(34).
Lawaridi lake jina ,
Watu wote walifana,
Angebebwa danadana,
Hoihoi itandapo.

(35).
Pa haki alikuwapo,
Japo hataki malipo,
Hangecharazwa kipopo,
Alipendwa kwa wemawe.

(36).
Alipenda kwa wenziwe,
Siti akasaidiwe
Hishima wakampawe,
Hadhi angeshushiwaje?

(37).
Mema yake wayataje,
Udaku kwake usije,
Huyo angepuuzwaje?
Sifa zi’kuwa dhahiri.

(38).
Siti banati Zuberi,
Mahafali kawa kheri,
Hewa kawa si ghubari,
Takirima ikafana.

(39).
Kenda walohusiana,
Chuo wakakongamana,
Usowe akauchuna,
Shahada akipatiwa.

(40).
Huyo alishangiliwa,
Si haba kafurahiwa,
Zawadi katunukiwa,
Huyo Siti Lawaridi.

(41).
Vema alijiadidi,
Mwanasheria abadi,
Alikuwa hana budi,
Alijiona wakili.

(42).
Aiguse serikali,
Matatizo akabili,
Afwate sheria kali,
Apate ukakamavu,

(43).
Angeisha unyamavu,
Punde aseme kwa mbavu,
Alete upeketevu,
Japo fujo hakutaka.

(44).
Gauni kajipachika,
Lawaridi kasifika,
Jioni katawanyika,
Walokuwa mahafali.
(45).
Kahuzunika wavuli,
Walompenda wakili,
Kuogopa yake hali,
Walimuona mahiri.
(46).
Huzuni kwa wahadhiri,
Kwachwa na biti Zuberi,
Dhambi aliyejibari,
Rabuka alimwogopa.

(47).
Wake moyo alijipa,
Wazo hakutapatapa,
MAbaya alipokwepa,
Ukata si ulemavu!

(48). 
Vumilivu hula bivu,
Japo huna upotovu,
Subira si upumbavu,
Usidanganywe na mtu.

(49).
Hakudhihakiwa katu,
Wenye akili fugutu,
Kwake wakawa na utu,
banati mwanasheria.

(50).
Si haba walimwambia,
Waliomsimulia,
Sifa wakampatia,
Siti Lawaridi mwema.

(51).
Katu kawapa huduma,
Michomo yao kusema,
Walimu kwa wakulima,
Haki zao kutetea.
(52).
Kote utu kaenea,
Ufisadi kakemea,
Wema ukaendelea,
Ya waroho nchi yao.

(53).
Siti katosheka moyo,
Sana karembeka huyo,
Kapendeka asemayo,
Wengi yakawavutia.

(54).
Wengi jeki kawatia,
Hao waliofifia,
Amara kawapatia,
Fedha alikuwa nazo.

(55).
Wasokuwa na uwezo,
Walokuwa na vikwazo,
Kwao kawa liwazo,
Tajiri wenye ndarama.

(56).
Fedha nyingi kamwandama,
Kitongojini kahama,
Kenda mtaani Wima,
Lipi lingemsumbuwa?
(57).
Mchanga alivvyokuwa,
Fedha kwake zilituwa,
Vya thamani kanunuwa,
Lawaridi kakwasika.

(58).
Ekosa kusikika,
Kijiji kukikumbuka,
Mtaani kasifika,
Mwanasheria ajwadi!

(59).
Sheria kaishadidi,
Ishadidike abadi,
Kwimarika ikadi,
Alikuwa na idili.
(60).
Redioni alikuli,
Runingani si kalili,
Magazetini mawili,
Likawa jambo shuruti.

(61).
Banati Zuberi Siti,
Kaufanya utafiti,
Kawa kama fashisiti,
Wavyele wakamkosa.

(62).
Kuonekana kwa kisa,
Kijijini alikosa,
Kwa rununu alijisa,
Hangepata muda kwenda.

(63).
Mabaraza kayaunda,
Kuko huko alishinda,
Ya haki akiyatenda,
Alipenda uzalendo.

(64).
Wazazi kawa mkondo,
Kakomesha lao pendo,
Kwa hayo yake matendo,
Kutumikia taifa.

(65).
Alipandishwa wadhifa,
Aangamize maafa,
Kwa hayo yake maarifa,
Popote alipendeka.

(66).
Alitamani hakika,
Pasipo kufadhaika,
Kusoma bila kuchoka,
Ndo maana kenda ng’ambo.

(67).
Nchi hiyo ya umombo,
Vema angejua mambo,
Ajue za ng’ambo nyimbo,
Punde awapo msomi.

(68).
Kwa masomo kujihami,
Etaka shahada kumi,
Japo hakuwa mlimi,
Ng’ambo kasoma makini.

(69).
Hakuupenda utani,
Kuingia vitabuni,
Ilikuwa ndo kanuni,
Kusoma kwa utulivu.

(70).
Katu hakuwa mvivu,
Esoma kwa uangavu,
Hizo bongo zake pevu,
Kaishi ughaibuni.

(71).
Kawa ulaya chuoni,
Sheria kuwa wazoni,
Liposoma vitabuni,
Nchi hiyo ya ulaya.

(72).
Kapewa nyingi hidaya,
Tele kumtunukiya,
Hadi ilipowadiya
Kurudi kwao nchini.

(73).
Akaabiri ndegeni,
Fikira nyingi wazoni,
Kielekea nchini,
Sheria kuisukuma,

(74).
Serikali kaegemea,
Kaikomesha husuma,
Hakujawa na tuhuma,
Lliyapenda mazuri.

(75).
Akavuma umahiri,
Siti asiye ghururi,
Alitoa tahariri,
Baya likiongezeka.

(76).
Nchini alipendeka,
Kwa misitu na kwa nyika,
Huko kote kasifika,
Sifa nyingi maridhawa.

(77).
Kwa wengi aliambiwa,
Bungeni ngechaguliwa,
Kiti kinapogombewa,
Alipendwa sana kote.

(78).
Siti hatamu apate,
Uchaguzini apite,
Achaguliwapo kote,
Biti Siti wa Zuberi.

(79).
Alikuwa nayo kheri,
Mema aliyahitari,
Aliishuku hatari,
Maovu hakuyataka.

(80).
Uchaguzi ulifika,
Lawaridi kapendeka,
Sifa zake kasikika,
Akawa mbunge kwao!

(81).
Akawa yeye yu ngao,
Kwa hao wasumbukao,
Kafiri na waombao,
Banati Siti Zuberi.

(82).
Kateuliwa waziri,
Miswada alihariri,
Akaitia mihuri,
Yake Wizara ya Haki.

(83).
Mengi aliyahakiki,
Kutetea nyingi haki,
Kwa wale hawasikiki,
Kazi nyingi kamkumba.

(84).
Nchi yote akatamba,
Watu wote kawapamba,
Alianza kujigamba,
Sana aliposifika.

(85).
Tabiya kabadilika,
Yeyote hakumtaka,
Hata wa yake marika,
Kaanza kuwapuuza.

(86).
Ya ujinga kauliza,
Yaso haki katangaza,
Wazazi kawapuuza,
Hao walofukarika.

(87).
Wazazi waliteseka,
Moyoni waliudhuka,
Hao walisononeka,
Wazazi wake waziri.

(88).
Hiyo haikuwa siri,
Wengi waliyahubiri,
Maovu yake waziri,
Madaha ya bi ‘tausi’,

(89).
Alikuwa na fulusi,
Hizo si haba kiasi,
Si wachache zilighasi,
Za bure zake ndarama.

(90).
Huyo kakosa heshima,
Naye kapata lawama,
Toka kwa baba na mama,
Wazazi walomleya.

(91).
Huzuni ikamwendeya,
Kukosa kunyenyekeya,
Ya wema kuwatendeya,
Akaanza kupumbaa.

(92).
Akili zikalemaa,
Bongo kutu zikajaa,
Bunge wakamkataa,
Bungeni kasimamishwa.

(93).
Watu wengi wakatishwa,
Kimako kwao kapashwa,
Nyoyo zao waliwashwa,
Kumwona huyu wazimu.

(94).
Yeyote hangemlaumu,
Yeyote hangemheshimu,
Ilikuwa ni nujumu,
Waziri mwenye kichaa.

(95).
Lawaridi kapumbaa,
Habari zikazagaa,
Popote zikatangaa,
Kama wingu zilitanda!

(96).
Mji alirandaranda,
Mitaani alishinda,
Ya soni alitenda,
Matambara akivaa.

(97).
Mitaani alikaa,
Kutuliya kakataa,
Hilo lilikuwabaa,
Lililotanda nchini.

(98).
Aliomba mitaani,
Mararuraru mwilini,
Bila kiatu guuni,
Ilikuwa raha yake.

(99).
Kalia wazazi wake,
Kilio kikasikike,
Moyoni wakaudhike,
Daima walihamaki.

(100).
Mitaani alibaki,
Huyo mtetea-haki,
Popote akijinaki,
Lawaridi kunyauka!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*