Wanapoingia jandoni, ni tarajio la kila mtu kwamba watatoka wakiwa na hulka zinazoandamana na mienendo wa wanadamu wanaoithamini taathima. Je, huo ni ukweli? Soma shairi hili linalofafanua mengi. Upujufu Jandoni


Upujufu Jandoni

Walio moja hirimu, vioja vingi huona,
Wawafunzao nidhamu, wakijifanya mitwana,
Hudhaniwa waadhamu, wagigisi wa fitina,
Uharibuo nidhamu, ni upujufu jandoni.

Mwawaona wafadhili, wafawidhi wa jandoni,
Fadhili zao kalili, wawaonyao kaini,
Dhana zao za ukali, kuwafundisha halani,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Kwangu wanikereketa, wajifanyao wajuvi,
Ghulamu wakilengeta, kuzitosheleza ngovi,
Vijana hulishwa mwata, mawaidha ja viwavi,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Upotovu hupakiwa, ya ngono ndo anwani,
Nidhamuyo kuumbuwa, uchafu uso kifani,
Majando wao hutuwa, machweo bila idhini,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Wafawidhi wa majando, wote wawe waongofu,
Wasiwe na ukaini, tabiazo ziwe nyofu,
Wasije kuwa haini, wahainio wanyofu,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Yote kwa kuwaambiya, nidhamu iwe lisani,
Wanamajando kugaya, wasiweze majandoni,
Wasiwe wa kukisiya, maishayo mashakani,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Hadhari mbele hatari, nidhamu iwe jandoni,
Tusije kutahayari, ichafukapo hisani,
Wavaao kanchiri, ghulamu wasiwahuni,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Ya vidosho maanani, ambayo hufasiliwa,
Yao siti mawazoni, hayo yote kuondowa,
Wayajue ya lisani, kwao ngono yalorowa,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Tisia natamatiya, dhana yangu ya muhimu,
Dhahiri nimewambiya, jando iwepo nidhamu,
Itande njema tabiya, tusichafue nidhamu,
Uchafuao nidhamu, ni upotovu jandoni!

Taifa Leo: Juni 11, 2006

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*