Usinidharau kwa sababu ya kazi yangu. Yawache yangu nami nisishughulike na yako. Tuwapo kazini, kila mtu ni kwa sababu ya riziki yake. Usinibeze


Usinibeze

Nitakapokukanziwa, hutaki kunikanziya,
Wanuna ukiambiwa, surwa hutaki kutiya,
Bariyo ndiyo wagawa, hutaki kunipikiya,
Mpishi usinibeze, sijawa kazini nile.

Wadinda kunipakua, wangoja kiwe utando,
Wanipa kichoungua, unipakulie vundo,
Kuniudhi warajua, udhia wako mkondo,
Mpishi usinibeze, sijawa kazini nile.

Kichujio hutumii, chai inayo majani,
Vema hunipakulii, masizi kwenye sahani,
Hicho huniandalii, kiandalike mezani,
Mpishi usinibeze, sijawa kazini nile.

Usinipe jicho baya, niingiapo garini,
Mabaya kuniambiya, nikaliapo kitini,
Tazama vizuri giya, uushike usukani,
Dereva usinipuze, sipo kazini nibebwe.

Kioo cha nje ona, ajali ukaichunge,
Usukani kukazana, safari yetu tuifunge,
Mafuta kanyaga sana, yaache yako mazonge,
Dereva usinipuze, sipo kazini nibebwe.

Barabara ufuate, bila mchomo moyoni,
Mengine usiyapite, uyakutayo njiani,
Tu waja wa Mola sote, wabeba wengi garini,
Dereva usinipuze, sipo kazini nibebwe.

Shika vipeto vizuri, barua peleka vema,
Tarishi usisubiri, utumwapo nenda hima,
Zikishapigwa muhuri, upeleke kwa hishima,
Tarishi usinitweze, sipo kazini utumwe.

Uendapo usiende, kwangu miye ni mamoja,
Vichochoroni ushinde, haraka udinde kuja,
Silazimishi utende, sidhani ni yangu haja,
Tarishi usinitweze, sipo kazini utumwe.

Huduma yako sitaki, katu sitapatiliza,
Mwenyewe ninazo haki, kamwe hutanipambaza,
Silifanyi lamikiki, pumuwa kupeleleza,
Tarishi usinitweze, sipo kazini utumwe.

Endapo nimekosea, unisamehe topasi,
Japo sitanyenyekea, mwenyewe nikikughasi,
Nikikkorowezea, kaziyo ni utopasi,
Topasi usinibeze, sipo nende msalani.

Ni mwekundu mstari, sipofanya kazi yako,
Kufanya bidii kheri, ili ikipate chako,
Tuuone uhodari, kule kazi ufanyako,
Topasi usinibeze, sipo nende msalani.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*