Watakutenga na wakudharau.Baki tu na Muumba wako. Muombe na umtegemee kwa lolote. Kama vile mama tasa huomba na kubarikiwa kupata mtoto. Usiye na Mwana


Usiye na Mwana

Hili langu ni liwazo kwa wagumba walomaka,
Hili langu ndilo wazo, kamwe hutapapatika,
Rabana awe mwongozo, maisha kulainika,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Moyo piga konde mama, vishindo stahimili,
Kupiga wako mtima, jaskamoyo usijali,
Fukuto si kuloloma, na kamwe si ujahili,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Kweli ufikapo mwisho, mwanzo mpya utapata,
Usijivike kitisho, simama kwa kujikita,
Hili langu hakikisho, mwana halali tapata,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Uso wako kuuchuna, sali pasi na fedheha,
Mkabala na Rabana, na usiwe wa karaha,
Mtimao kwa upana, kamwe siwe na kariha,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Ushunge yako hamaki, yeyote kumshutumu,
Sali pasipo mikiki, akurehemu Rahimu,
Baina ya halaiki, ni wako huu msimu,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Kiwewe chako ni mwana, kutunga uja uzito,
Juhudi ukimimina, zote zaungua moto,
Akujasiri Rabana, upate wako watoto,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Kumbuka Sara na Hana, walinyakua baraka,
Jitimai yao wana, Rabana kawakumbuka,
Mlingane Maulana, baraka atakuvika,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Kwa kudura za Rabana, hapana budi kishindo,
Ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo,
Mfuate Maulana, kwa mema yako matendo,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Kikomo ndipo nafika, nimeyakadiri,
Abadi kugadhibika, yako mawazo ghairi,
Kaburini kuyazika, atakulinda Kahari,
Usiye na mwana omba, Rabana akurehemu.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*