Hulazimishwi kuamini. Abudu Mungu unayemwamini. Mshukuru Mungu kwa lolote maishani. Waaminio Amini


Waaminio Amini

Heri walio wanyofu, na wasalio Masihi,
Katu waso unyarafu, Rabana wasifedhehi,
Huratibu uraufu, sifa zao zi wajihi,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Walio njema gharadhi, na gere wasioona,
Nyoyo zao kukabidhi kwake Mwenyezi Rabana,
Maulana mwenye hadhi, Kahari hatawakana,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Wasio na majisifu kwao hawana ghururi,
Nyoyo zao ni kunjufu, na kamwe hawaghairi,
Daima wafurahifu, simanzi hawafikiri,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Makadara huwakifu, waja waliomwamini,
Huduma yake Latifu, ukombozi hawahini,
Kamwe si walaanifu, wokovu wao leseni,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Mwenyezi huwaghofiri, wamwaminio Mwokozi,
Wale wote wakikiri, nguvu tena huwajazi,
Huongozwa na Kahari, jabari la ukombozi,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Walio na maadili, huwa nyingi zao sifa,
Wokovu wao ni nguli, ukifuo maarifa,
Wema wao si kalili, udhihirishao sifa,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Wafanyao kwa lilahi, zao ni nyingi baraka,
Watukuzao Ilahi, na wasomao nyaraka,
Wamwaminio Masihi, huduma kutukutika,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Barakazo hukolea, na  kudurs kujihsmi,
Wasiweze kuotea, walio potovu vumi,
Wasije kunyemelea, waishio kwa kinyemi,
Waaminio amini, kwangu mie naamini.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*