Hukosi mjuaji. Kila jambo analijua. “Ujuvi wake waudhi, hakunalo halijuwi!” Ujuvi Wake Waudhi


Ujuvi Wake Waudhi

Amejipandisha hadhi, hakunalo haumbuwi,
Tabiaze haziridhi, kwangu mie sivutiwi,
Cheo amejikabidhi, akadhani sigunduwi,
Ujuvi wake waudhi, hakunalo halijuwi!

Ayajua ya lafidhi, nitamkapo sijuwi,
Siku ya leo yu kadhi, kesho azoa mabiwi,
Haja yake kujikidhi, hakunalo hakosowi,
Ujuvi wake waudhi, hakunalo halijuwi!

Imenijiya ghaidhi, nisibaki sidopowi,
Akose haombi radhi, unyenyekevu hatowi,
Hatojuwa abughudhi, tabiaze hagunduwi,
Ujuvi wake waudhi, hakunalo halijuwi!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*