Shairi hili linaibua mazungumzo kati ya Kimani wa Mbogo na Muna Moon Ahmed kuhusu masuala ya mapenzi, thamani ya ndoa, na sifa za kuwa na hishima mwenyewe na katika jamii. Kimani anazungumzia kuhusu vazi la Muna na jinsi linavyopunguza heshima yake mbele ya jamii. Muna, kwa upande wake, anajibu na kumueleza Kimani kuhusu thamani yake, imani yake, na matumaini yake ya baadaye. Ningekupenda Ungevaa Rinda


Ningekupenda Ungevaa Rinda

Kimani wa Mbogo:

Mahaba ningekudenda, kukupenda singedinda,
Mapenzi ningeyaunda, nikutunze kama kinda,
Sipendi yako magwanda, yaso mema wayatenda,
Banati ningekupenda, ungekuwa nalo rinda!

Huba nafanyia inda, usidhani utashinda,
Sifa mbovu zimetanda, uchi wako ni ajenda,
Hujioni umekonda, utulie kutoranda,
Banati ningekupenda, ungekuwa nalo rinda!

Ukijiandaa kwenda, huna mama kukulinda,
Wadhani tunazipenda, kuvaazinazoganda,
Huna lako moja rinda, la hishima lilowanda,
Banati ningekupenda, ungekuwa nalo rinda!

Unadhani unapanda, umbo lako kuliunda,
Moyo wako hutodunda, ukwoneshe la kutenda,
Hakuna wa kukuwinda, hupendeki zote nyanda,
Banati ningekupenda, ungekuwa nalo rinda!

Twakuona u kidonda, unavyozipanga inda,
Kokote unakoenda, unatafuta mabunda,
Usidhani umeshinda, kuvaa lisilotanda,
Banati ningekupenda, ungekuwa nalo rinda!

Muna Moon Ahmed:

Mie sijadinda, bado nakutamani,
Bado ni kinda, sijakolea jamani,
Mzazi anilinda, ye wa zamani,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Kabla kunitunda, siseme faraghani,
Moyo takudunda, ufe taabani,
Sitafuti wa Runda, marejeo ni ngamani,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Wasojua kupenda, yanawawashiani?
Fikra za punda, umbea wathamini,
Hawakutakii nyonda, ila tu kunikhini
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Penzio ni bunda, kwa haya amini,
Umepata chanda, roho ilojaa imani,
Sitokuvika sanda, nafuata la mwadhini,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Kwangu hutakonda, sikuati asilani,
Mwalimu tajibonda, nisubiri ewe Kimani,
Katu sitokutenda, sitokugeuza kuni,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Ye anipiga randa, nilimkoseani?
Alinunua kitanda, katoroka wake hani,
Amfate Rwanda, alikotorokeani,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Siwi kandanda, nikachezwa uwanjani,
Sijaikataa kibanda, ulonijengea shambani,
Penzi halijaganda, likajaa ghalani,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Ingawa wanipenda, takueleza walakini,
Inofaa hebu tenda, njoo kwetu nyumbani,
Wangoja parapanda, itokayo binguni?
Natafuta rinda, n’subiri mwandani

Wapiga kinanda, kunielekeza dhambini?
Mbegu tukipanda, wazazi tanilaani,
La kuu ajenda, kuitimiza dini,
Natafuta rinda, n’subiri mwandani.

Nami mekupenda, wangu namba wani,
Kwangu hutokonda, waache washindani,
Takuchezea kanda, upatapo idhini,
Nitanunua rinda, n’subiri mwandani.

© Kimani wa Mbogo (30/04/2010)

Kimani wa Mbogo:

– Kimani anaelezea jinsi angependa kumpenda Muna ikiwa angevalia kwa heshima zaidi na kujistahi.
– Anamtahadharisha Muna dhidi ya kuvalia nguo ambazo zinamfanya aonekane kama hana heshima mbele ya jamii.
– Anakosoa mtindo wa mavazi ya Muna, akisema haidhuru yeye mwenyewe lakini inawadhoofisha wengine.
– Anasisitiza kwamba Muna hajapata yeyote anayemthamini kutokana na mavazi yake na tabia zake.
– Kimani anamwonya Muna dhidi ya kujiona mwenye thamani na kumtaka atafakari upya kuhusu thamani yake mwenyewe.

Muna Moon Ahmed:

– Muna anajitetea kwa kusema bado ni kinda na hajakomaa kabisa.
– Anasema anaendelea kutafuta “rinda” – labda kuashiria vazi la heshima au mwandani wa kweli.
– Anamjibu Kimani kwa kusema hatafuti mtu kutoka sehemu fulani maalum na yeye bado anamsubiri.
– Muna anaeleza kuwa wapo wengi wanaompenda, lakini wanataka kumgeuza na kumfanya afuate njia zao.
– Anasisitiza imani yake katika dini na anamwomba Kimani aje kwake nyumbani.
– Anachukizwa na wale wanaomkosoa na kumtaka afuate njia zao bila kuelewa thamani yake halisi.
– Anasisitiza upendo wake kwa Kimani na kutaka kuheshimu mapenzi yao.

Shairi hili linaonyesha mawasiliano kati ya wapenzi wawili ambao wana mtazamo tofauti kuhusu mapenzi, heshima, na jinsi ya kuonyesha upendo. Licha ya tofauti zao, wote wanatafuta kuwa na mahusiano yenye heshima na kuelewana. Wanatafuta maelewano, heshima, na kutambua thamani ya kila mmoja wao katika uhusiano wao.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*