Msiziwanie hadhi, mkibusu ufahari,
Huenda mkabughudhi, magwiji wa ushauri,
Walisema heri radhi, mali sana huwa shari,
Pasipokuwa arudhi, tungo haiwi shairi!
Hata upambe lafudhi, kwa lahaja ziwe shwari,
Wasomao utaudhi, usipofata bahari,
Tungo za haja kukidhi, zazuia kushamiri,
Pasipokuwa arudhi, tungo haiwi shairi!
Zipashe hizo nyaadhi, ila muhimu urari,
Wadai yetu upudhi, kaamua kughairi,
Hizo walitukabidhi, ndizo zenye uhodari,
Pasipokuwa arudhi, tungo haiwi shairi!
La kuitwa mfawidhi, si maana kufahiri,
Utungayo ni maradhi, kupooza ushairi,
Iwate hiyo ghaidhi, uanze kutafakari,
Pasipokuwa arudhi, tungo haiwi shairi!