Ni wakati wa washairi kuwa makini ili kutetea fani ya ushairi. Wengine wametunga mengi yasiyofuata arudhi wakiyaita mashairi. “Pamoja tuunganeni, tuokoe ushairi.” Tuokoe Ushairi


Tuokoe Ushairi

Nimeshakisia shari, tena hofu ukumbini,
Sijatunga kubashiri, ila natoa maoni,
Badala ya kushamiri, yatokota hino fani,
Pamoja tuunganeni,  tuokoe ushairi.

Kushindana umahiri, wa sasa wanatamani,
Wanatungia fahari, vina ovyo na mizani,
Hawajali ya bahari, na vina havifanani,
Pamoja tuunganeni,  tuokoe ushairi.

Magwiji wameghairi,  kutunga kama zamani,
Nayakumbuka mazuri,  enzi hizo kutamani,
Walizipamba kwa zari, tungo walizozibuni,
Pamoja tuunganeni,  tuokoe ushairi.

Tutungie yanojiri, tuwate ya kufitini,
Usitungie dinari, lengo likiwa mapeni,
Sipanie uhodari, ya kutunga hubaini,
Pamoja tuunganeni, tuokoe ushairi.

Tukubali ushauri, yajayo masikioni,
Mengi yameuathiri, lugha zao mitaani,
Twataka la kunawiri, pembe zote duniani,
Pamoja tuunganeni,  tuokoe ushairi.

Lijapo la tahadhari,  tulipate kwa makini,
Tuzieneze habari, vyomboni hata shuleni,
Tuutakie la kheri, ushairi kuthamini,
Pamoja tuunganeni,  tuokoe ushairi.

Muhimu kutabasuri, tufanyapo la kughani,
Tuamue tafakuri, tukitunga vitabuni,
Tutafiti kuhadhiri, tukomeshe walakini,
Pamoja tuunganeni,  tuokoe ushairi.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*