Usinidharau kwa kunitazama tu. Unavyoniona kama sifai, wapo wengine wanaoujua wema wangu. Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  Wengine Wanitamani!

Wengine Wanitamani!

Wanibeza kwa hujuma, bila la kunithamini, 
Mara kwa zako tuhuma, za kuonesha sifani, 
Kejeli zinaandama, kunifanza niwe duni, 
Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  

Sikosi la taadhima, kwa hilo ulithamini, 
Si kwa mabaya kuvuma, siseme zuri sinani, 
Ola mambo kwa hikima, ulipate la kughani, 
Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  

Kusaili utakwama, uwe na la walakini, 
Kilele chako hatima, ukweli ukibaini, 
Yapo mengi kama dhima, si yote ya kulaani, 
Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  

Unavyozidi kuhema, halijawa la utani, 
Kinyongo kukuandama, la kwangu huliamini, 
Mekosa hata rehema, i tukizi maishani, 
Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  

Uwapo na la neema, si kwamba una amani, 
Haiwi hivyo daima, hali yako aushini, 
Sijakikosa cha wema, tena nina tumaini, 
Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  

Nimefika kaditama, uwazi sijakuhini, 
Beti sita nimekoma, ujumbe upo nyumbani, 
Likomeshe la lawama, utende mema mwandani, 
Ni kwako sina la wema, wengine wanitamani!  

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*