Je, umewahi kufikiria nchi bila ukabila, ubaguzi au uhasama? Wakati nchi yetu itakuwa na amani ndivyo wazalendo wataifurahia haki yao na kupendezwa na uzalendo wao. Tuudumishe Umoja


Tuudumishe Umoja

Jukwaani twaingia, tutoe wetu uneni,
Tusibaki kutulia, utulivu kutamani,
Msiwe mwaangamia, kizazi kukilaani,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Wakenya tunaumia, mara hakuna amani,
Ukabila tunalia, wengine kufanywa duni,
Hamjui ni hatia, ubaguzi kuubuni,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Limekuwa la udhia, tofauti ya imani,
Dini yako wasifia, za wengine huthamini,
Jueni zote ni njia, kuelekea mbinguni,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Penye nia pana njia, tufanye yote makini,
Ukabila kufifia, tuweze kujiamini,
Mengi yanapotukia, kwa Mungu ni shukurani,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Wakenya twajivunia, si haba humu nchini,
Sifa tumejipatia, kwa mengi tunayobuni,
Mengi tukiangazia, la muhimu ni amani,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Twatazama asilia, rangi, kabila na dini,
Baadaye twajutia, athari tusizodhani,
Mbali twawatupilia, waja kuwafanya duni,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Jiepushe kuchukia, amani ukabaini,
Tuishi kufurahia, tupendeze maishani,
Mwenyezi akiridhia, tutakuwa washindani,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Hatima twatamatia, hoja zetu za thamani,
Twadhani mmesikia, mwaelewa kuamini,
Mengine yafuatia, tuyajue kwa undani,
Tuudumishe umoja, utu na utengamano.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*