Hamnazo mwajitia, nipendaye mwabubuta,
Vya wengine mwasifia, kilicho chake mwabeta,
Lawama mnamtia, ikawa mnamsuta,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.
Mema yanapowadia, mwaona yenu yasita,
Lake mwaita hatia, kwa yenu mnajibwata,
Mwadhani mmetimia, mkajiona mwakita,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.
Dada yuwalialia, amebaki akibweta,
Tanuri ameingia, mtashangaa kupita,
Thamani mwakadiria, msijue awaketa,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.
Maovu mwamtajia, dada mwamkereketa,
Lake hamjasikia, moyo mnavyofukuta,
Pale mnapopitia, kutwa mtajikunyata,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.
Kwa mengi mwajisikia, ati bongo amenata,
Majina mwampatia, hamna radhi kumwita,
Laana mwamtakia, kumwingiza kwa matata,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.
Yenu sitakubalia, mtakavyo kumng’ata,
Matusi kumvamia, si jambo la kumgota,
Sasa mnafurahia, vibaya kumkong’ota,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.
Adhabu itasalia, vitukuu kufuata,
Mungu atamjalia, kwa huo wake utata,
Yote mnamfanyia, yanamfanya kukita,
Sijali mnavyomwita, kwangu huwa maridhia.