Ndoa ni jambo la muhimu linalostahili hekima na busara. Ni jambo linalofaa na kustahiki uaminifu. Mheshimu, mtunze na umfae. Mke Unaye Nyumbani


Mke Unaye Nyumbani

Utunzi wa Kimani wa Mbogo | Sauti ya Victor Mulama

Hujawata ya utani, watu wakafurahia,
Awaye huwa mwandani, awe akukumbatia,
Umekwama mawazoni, dunia kujijulia,
Mke unaye nyumbani, wengine wawatania.

Akufaaye humwoni, pingu uliyemtia,
Imekuwa hakwamini, kila muda yuwalia,
Hukwandalia jioni, chakula kakupikia,
Mke unaye nyumbani, wengine wawatania.

Huna lako la kuhini, mapeni huwapatia,
Hulikosi la kubuni, hoja kumumiminia,
Hujua unavyodhani, hukosi kujisifia,
Mke unaye nyumbani, wengine wawatania.

Una mengi ya undani, hukosi kuhadithia,
Waonyesha hadharani, unavyowasimulia,
Hujawa nalo la soni, yale unatufanyia,
Mke unaye nyumbani, wengine wawatania.

Hukosi yako imani, vile wajiangazia,
Umekosa la makini, kwa hilo kujitapia,
Waingia baharini, jambo la kujitakia,
Mke unaye nyumbani, wengine wawatania.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*