Unapoliona wingu jeusi, si maana kwamba mvua itanyesha. Inapoiona dalili, si lazima iwe ishara ya jambo fulani kutendeka. Ukweli huu unadhibitishwa na shairi hili. Wingu Jeusi Kutanda

Wingu Jeusi Kutanda

Utunzi wa Kimani wa Mbogo | Sauti ya Victor Mulama

Usione unatenda, ukadhani una mema,
Si la shuruti kushinda, ni baraka kukwandama,
Haliwi unalopenda, ila kwa nyingi neema,
Wingu jeusi kutanda, kunyesha si kwa lazima!

Mada unazoziunda, haziwi bila hekima,
Kunawiri zitadinda, ingakosa taadhima,
Kila mwendo unakwenda, papo yu nawe Karima,
Wingu jeusi kutanda, kunyesha si kwa lazima!

Ngoma unapoidunda, huwa muhali kuvuma,
Ufundi wako ni inda, unaiathiri wema,
Hadhi huwezi kupanda, ungaharibu huduma,
Wingu jeusi kutanda, kunyesha si kwa lazima!

Ungaliandaa gunda, kwa fyekeo na kulima,
Hutabaki kwa kitanda, ikakwandama lawama,
Unapolitaka tunda, utafanya la ujima,
Wingu jeusi kutanda, kunyesha si kwa lazima!

Halikosi la kurunda, ukisubiri uzima,
Mola ndiye hutulinda, inapokuwa tuhuma,
Mwovu anapotuwinda, juhudi zake hukwama,
Wingu jeusi kutanda, kunyesha si kwa lazima!

Binadamu hawi kinda, akalishwa kwa mtama,
Kushuka hadi kupanda, hazikosi na hujuma,
Maishani si mabunda, kiyapata himahima,
Wingu jeusi kutanda, kunyesha si kwa lazima!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*