Peke yako hutaweza bila kuungana na wenzako. Hivi ni sawa na vile jiwe moja haliinjiki chungu. Usijitie hamnazo mambo ya mwenzako. Huenda ukamhitaji. Shirikiana na wengine, uwafae nao wakufae. Moja Haliinjiki Chungu


Moja Haliinjiki Chungu

Kwa sasa ninayo hoja, hata kama ya uchungu,
Nimeviona viroja, vinavyokutia pingu,
Maswahibu huna haja, umepotea mwanangu,
Figa hilo lako moja, litainjikaje chungu?

Twajua wako uteja, wenendako wanguwangu,
Maneno unayotaja, yamekithiri mizungu,
Kwa jamii wajichuja, huthamini hata Mungu,
Figa hilo lako moja, litainjikaje chungu?

Mambo kweli ni kangaja, huja pia kwa mikungu,
Unahitaji daraja, kivuko kama cha pungu,
Kwa wanadamu hujaja, wajificha kwa vitangu,
Figa hilo lako moja, litainjikaje chungu?

Litakwalo ni umoja, ili pako pawe pangu,
Umezidiwa na luja, ukabadilika bungu,
Ishi vema nao waja, usiishi zako mbingu,
Figa hilo lako moja, litainjikaje chungu?

Hiyo yako si faraja, ni mateso chunguchungu,
Uzipatapo wafuja, unenewapo u nungu,
Upatacho wabigija, ukituonesha tungu,
Figa hilo lako moja, litainjikaje chungu?

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*