Wataalamu wana mengi. Huonyesha wakiwa nazo tarakimu ya kiongozi atakayechaguliwa kutawala. Wengine hulipwa kutengeneza takwimu zisizokuwa na msingi wowote wa kitaalamu. Ukweli ni upi? Wachaguzi na debe! Debe Ndilo Uamuzi


Debe Ndilo Uamuzi

Mna la hila wajuzi, tena hatuwaamini,
Zinakera zenu kazi, mwatangaza ya utani,
Tuisubiri mbawazi, mfanyavyo haifani, 
Hatuyataki maoni, debe ndilo uamuzi!

Ajuaye ni Mwenyezi, hayo yenu ni kubuni,
Tusubiri uteuzi, tutajua kwa makini,
Japo mnao ujuzi, mwatuingiza vitani,
Hatuyataki maoni, debe ndilo uamuzi!

Tukifanya uchaguzi, mtoe wenu uneni,
Hatutaki uchokozi, ghasia hatutamani,
Ya kero yatuyawezi, yaliyojiri zamani,
Hatuyataki maoni, debe ndilo uamuzi!

Mna wenu uchambuzi, yajayo hamuyaoni,
Ni bure ufafanuzi, mwaegemea fulani,
Angalipo kiongozi, takayeshinda mbioni,
Hatuyataki maoni, debe ndilo uamuzi!

Tuna pamba masikizi, vikwazo vimo machoni,
Yenu hayatupendezi, hayaleti la amani,
Yanatisha maelezi, kuchochea uhaini,
Hatuyataki maoni, debe ndilo uamuzi!

Ya haki hamtangazi, mwahadhiri yalo duni,
Vyenu ndivyo vizuizi, kwa wapendao imani,
Tumewajua kwa wazi, naliweka hadharani,
Hatuyataki maoni, debe ndilo uamuzi!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*