Hujui kemikali zinazotumiwa kutengenezea bidhaa na kurembesha. Wapo baadhi ya watu wanaosumbuka na kujuta kwa sababu nyuso zao zimebadilika wakitafuta urembo. Muwe Makini Mkirembeka


Muwe Makini Mkirembeka

Hizi rangi mwajipaka, kuchani na midomoni,
Mwajua zilikotoka, mzipate masokoni,
Zote zinazopakika, vema hazijulikani,
Yabidi mkirembeka, kujua muwe makini.

Fupi zisizovalika, kuonesha ya ugeni,
Wamfurahisha kaka, hujui yake maoni,
Baradhuli waoneka, upendaye ya kuzini,
Yabidi mkirembeka, kujua muwe makini.

Ya wengine ukitaka, piga bongo kwa undani,
Yawache ya kutukuka, ulivyo twakutamani,
Banati hueleweka, kwa mavazi ya mwilini,
Yabidi mkirembeka, kujua muwe makini.

Zote zinazotumika, haikosi walakini,
Yapo yametambulika, yanayoleta huzuni,
Vema yakafahamika, yangu mkiyaamini,
Yabidi mkirembeka, kujua muwe makini.

Huenda mwataabika, msijue kulikoni,
Lolote likifanyika, ulitie akilini,
Siha ukidhoofika, ujue kifo njiani,
Yabidi mkirembeka, kujua muwe makini.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*