Je, umewahi kujiuliza ni kwa nini nyuki huunda asali na bungo huunda udongo? Sote hatufanani. Umuhimu wangu si umuhimu mwa mwengine. Tafakari hayo! Nyuki Kuunda Asali

Nyuki Kuunda Asali

Tofauti taamuli, kilichoko kwenye bongo,
Ninazo zangu akili, unayo yako mipango,
Huluka ni mbalimbali, sio wote wa maringo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

Nitendalo ni la kweli, huenda lako uwongo,
Ninapolitenda hili, usiwe nacho kinyongo,
Maneno yangu kamili, kwako huwa songosongo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

Kipawa changu halili, si kama chako kitengo,
Urembo wangu wa hali, sio kama wako chongo,
Hayana jambo ya mwili, hatutofanana shingo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

Ninapozitunga kali, una tofauti tungo,
Ni kipana Kiswahili, kila mtu na mchango,
Hiki hakina mithili, hayafanani malengo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

Ufungapo kwa kufuli, mie sitofunga lango,
Ninapoyachunga mali, unatafuta kwa gongo,
Sheria ziwapo kali, kunao walao hongo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

Kunongesha nahimili, kumbe wewe na simango,
Utakuta ni’ wakili, wewe uwapo utingo,
Meno yawe si kalili, kwako wabaki kipengo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

Ninazo zangu shughuli, niyatimize malengo,
Yangu na yako ni mbali, hayalingani maungo,
Yupo asemaye kweli, kama vile yupo mwongo,
Nyuki kuunda asali, bungo huunda udongo.

© Kimani wa Mbogo (24/05/2012)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*