Watakusema na wakudharau lakini hayo hayatabadilisha maisha yako. Shairi hili linawashauri wenye tabia kama hizo kukoma na kushughulikia mambo yao binafsi. Lisome kwa makini. Nyumba Usiyoilala


Nyumba Usiyoilala

Jiepushe na aila, iso yako itengeke, 
Halikuhusu kabila, langu hilo usitake, 
Ningabaki kuwa fala, niache niathirike, 
Nyumba usiyoilala, huzijui ila zake! 

Ningayatunga makala, yawaje uhamanike, 
Isokuhusu halula, haifai uudhike, 
Anijuaye ni Mola, mwanadamu sihusike, 
Nyumba usiyoilala, huzijui ila zake! 

Sizitaki yako hila, ueneze mwanamke, 
Kila siku navyokula, hayakuhusu umake, 
Imekufika dhalala, domodomo yakutoke, 
Nyumba usiyoilala, huzijui ila zake! 

Ziache za kwangu ila, toka kwako zitoweke, 
Ungazifuata mila, ungeyaacha makeke, 
Kwengine unakoola, huhusiki mambo yake, 
Nyumba usiyoilala, huzijui ila zake! 

Udaku mekutawala, kwa watu usipendeke, 
Upuzi ni yako ala, maneno yaseleweke, 
Ungejivika jamala, kwa watu ukapendeke, 
Nyumba usiyoilala, huzijui ila zake! 

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*