Mapenzi ya dhati. Mistari ya mahaba. Banati ameamsha hisia za mshairi. Kuniamsha Hisia


Kuniamsha Hisia

Umenifanya kuwaza, kwa mambo waniambia,
Nitasema kutongoza, jambo sikutarajia,
Mahaba umenijaza, kwa rinda ulovalia,
Banati umeniweza, kuniamsha hisia.

Menibidi kunyamaza, yako kutafakaria,
Kwangu umejitokeza, mahaba kunitakia,
Kwa kweli umejikaza, vema kuniangalia,
Banati umeniweza, kuniamsha hisia.

Siti umejitokeza, bidii kunisifia,
Yako meniambukiza, kabaki najimakia,
Kumbe umenipumbaza, sinalo la kukwambia,
Banati umeniweza, kuniamsha hisia.

Rima nimejiingiza, mtegoni kuingia,
Kwa wema wanitukuza, na debe kunipigia,
Wasibiri miujiza, moyo nikakupatia,
Banati umeniweza, kuniamsha hisia.

Nendapo unadukiza, huko kunifatilia,
Kupendeka wanikwaza, pekeyo ukasalia,
Wasema nakuliwaza, kwa hizi zangu tabia,
Banati umeniweza, kuniamsha hisia.

© Kimani wa Mbogo (03/10/2012)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*