Iwapo hujatimiza ahadi zako kwa mtu, usizidi kuongezea ahadi. Ahidi na utimize ndiyo amri yenye thamani. Ahadi Zako Sitaki


Ahadi Zako Sitaki

Hima nimejitokeza, niweleze washabiki,
Siku zote nimewaza, kovu kwangu imebaki,
Ahadi ukiongeza, zote hazitimiliki,
Ahadi zako sitaki, kwa yote hujatimiza!

Usemalo hujaweza, kisema halifanyiki,
Kwa hadhi wajitukuza, unapoizua chuki,
Ni mengi umeeleza, yote hayaeleweki,
Ahadi zako sitaki, kwa yote hujatimiza!

Kwa hila umetuweza, wasema hatuudhiki,
Wapenda kuhanikiza, ikuzidipo hamaki,
Lako ni kuchachawiza, ukinitakia dhiki,
Ahadi zako sitaki, kwa yote hujatimiza!

Huna haja kuongoza, waja hawatwaaliki,
Tawala kimiujiza, mambo yako siafiki,
Unapenda kutangaza, kumbe hayatimiliki,
Ahadi zako sitaki, kwa yote hujatimiza!

Sitaselea kwa kiza, kidhani hubainiki,
Tena ukajitokeza, nitakulenga mikuki,
Habari tazieneza, uadui ukabaki,
Ahadi zako sitaki, kwa yote hujatimiza!

Kwa bidii tajikaza, nijipatie miliki,
Hata ukinieleza, utakuwa husikiki,
Kutambua nimeweza, kidhani hufahamiki,
Ahadi zako sitaki, kwa yote hujatimiza!

© Kimani wa Mbogo (03/06/2012)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*