Wapo baadhi ya watu ambao hawana hoja. Watarudia jambo moja kila siku bila ubunifu wowote. lisome shairi hili uelewe ukweli wenyewe. Hurudia ya Kitambo

Hurudia ya Kitambo

Natunga kufahamisha, barua iso mafumbo,
Huenda nikakupasha, uwe panya au tembo,
Sitafunga kwa bahasha, ikasomwe hadi ng’ambo,
Hurudia ya kitambo, ladha yalokwishaisha!

Hutunga yaso maana, yakikuishia mambo,
Husema bora kuguna, mishororo au wimbo,
Huhifadhi lako jina, kwa nakishi na mapambo,
Hurudia ya kitambo, ladha yalokwishaisha!

Huweka zako tungoni, kutafuta cha matumbo,
Huandika ukighani, tungozo zilizo kombo,
Za siasa na za dini, serikali na majimbo,
Hurudia ya kitambo, ladha yalokwishaisha!

Hujiundia sanaa, ukijihami kwa fimbo,
Tajionea balaa, wenendapo kwa viambo,
Hujajua kunyamaa, kwa hayo yako maumbo,
Hurudia ya kitambo, ladha yalokwishaisha!

Huko si kuerevuka, ukaling’amua jambo,
Endelea kujipaka, ukajitia urembo,
Kituoni nimefika, uviwate hivyo vyambo,
Hurudia ya kitambo, ladha yalokwishaisha!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*