Uainishaji wa Mashairi

Mashairi ya Kiswahili huainishwa katika bahari tofauti kulingana na mtindo, umbo au matumizi ya lugha. Pia huainishwa kwa kutazama mbinu mbalimbali za kiufundi ambazo washairi hubuni na kuandikia. Bahari za ushairi ni nyingi mno. Bahari moja huenda ikawa na mikondo au mitindo mbalimbali. Baadhi ya bahari ya ushairi zilibainika kwa mashairi ya kale tu. Hapa tumeelezea bahari za ushairi kwa kuzingatia mipangilio mbalimbali.

Mashairi yanaweza kuainishwa kwa kuzingatia urari wa vina katika kila mshororo au ubeti. Vina vilivyotumika katika shairi vitaitambulisha bahari ya shairi lenyewe.

Katika mashairi ya arudhi, mshairi huzingatia sana uwiano wa idadi ya mizani kwa kila mshororo. Shairi linaweza kutambulishwa bahari yake kwa mtindo wa mizani kama vile mtunzi alivyozipanga.
Shairi linaweza kuwa na kipande kimoja tu kwa kila mshororo, miwili au zaidi. Kipande cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha nne huitwa ukwapi, utao, mwandamizi na ukingo mtawalia. Bahari za mashairi zinaweza kuainishwa kwa kuzingatia vipande hivyo au mishororo yenyewe.