Werevu huwa na wingi wa busara. Ni muhali kuwapata wakifarakana au wakigombana. Tofauti zao husuluhishwa bila ghasia. Hukosi wengine wasiolielewa hili. Wapo wasioithamini heshima wala busara. Hufarakana pasi na sababu. Lisome shairi hili uelewe ukweli huu. Werevu Huelewana


Werevu Huelewana

Utunzi wa Kimani wa Mbogo | Sauti ya Victor Mulama

Wajinga hufarakana, wakawa wanagombana,
Watu wanaojuana,  heri kushauriana,
Msibaki mwapigana, muwe mnaskizana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Werevu watakutana, iwapo wamekosana,
Hunena wakionana, hawawezi kutwangana,
Huyanena ya maana, vizuri wakafaana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Wajinga hukimbizana, maneno kurushiana,
Nyusoni hutazamana, mate wakitemeana,
Mara wanaburutana, ama wakatusiana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Werevu hukusanyana, ili kujadiliana,
Wengine hutafutana, mawazo wakakuzana,
Hata wanapokosana, hutaona wakiwana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Wajinga haya hawana, kwa mabezo hujiona,
Huyahifadhi ya jana, maovu kukumbushana,
Nguvu zao humenyana, kwa ngumi wakachuana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Werevu watajuzana, za maana kipashana,
Njiani wakikutana, kwa amani hupishana,
Huoni wavurugana, hupati wanazozana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Wajinga hutambuana, tena huwa wafanana,
Ubwege huonyeshana, ubozi wakafunzana,
Kwa vita watakumbana, vibaya wakapambana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Werevu huliliana, tena hufarijiana,
Vema hushauriana, pamwe wakikongamana,
Pesa hukopesheana, ama wakalipiana,
Werevu ndio hunena, vema wakaelewana.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*